Header Ads

RATIBA YA MICHUANO YA LIGI KUU TANZANIA BARA ILIYOANZA LEO.

Ligi Kuu Tanzania Bara inaanza leo, ambapo timu 10 zitacheza ili kuanza kampeni za kuwania kutwaa taji la michuano hiyo.
Kwa sasa ubingwa huo unashikiliwa na Yanga, ambao katika msimu uliopita wao ndio waliibuka washindi baada ya kufikisha pointi 73, huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Azam FC, walioshinda kwa jumla ya pointi 64.
Katika mechi za leo mabingwa watetezi, Yanga haitaweza kucheza dhidi ya JKT Ruvu na kulazimika  kuucheza mpira huo Agosti 31 ili kuiwezesha Yanga kuhitimisha mchezo wake wa Kombe la Shirikisho la Afrika dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo utakaofanyika Jumanne. Timu hiyo inaondoka kesho.
Yanga imeshindwa kukidhi vigezo vya kuingia nusu fainali kwenye michuano hiyo baada ya kupokea vipigo mfululizo kutoka kwa TP Mazembe bao 1-0 katika Uwanja wa Taifa, kabla ya kufungwa tena na bao 1-0 na Mo Bejaia huku wakichukua kipigo kingine kutoka kwa Medeama cha mabao 3-1.
Mechi za fungua dimba zitakazopigwa leo ni Simba ikiwakaribisha Ndanda katika Uwanja wa Taifa, Stand United itamenyana na timu iliyopanda daraja ya Mbao FC kwenye Uwanja wa Kambarage Shinyanga, wakati Mtibwa Sugar itaivaa Ruvu Shooting kwenye Uwanja wa Manungu na Majimaji ‘Wanalizombe’ watawakaribisha Maafande wa Tanzania Prisons ya Mbeya.
Upinzani mkali unatarajiwa kuwa kwenye timu za Simba, Yanga na Azam ambazo zinawania nafasi ya juu kileleni kwenye ligi hiyo ambayo inachezwa kwa mara ya 51 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1965.
Klabu 16, ukiwa ni pamoja na tatu zilizopanda daraja zitaungana na 13 zilizosalimika kwenye ligi iliyopita, zitachuana kuwania taji hilo ambalo kwa sasa linashikiliwa na mabingwa wa kihistoria wa ligi hiyo, Yanga. Yanga ndiyo klabu iliyotwaa mara nyingi ubingwa wa ligi hiyo tangu mwaka 1965, ikitwaa mara 26, huku wakifuatiwa kwa mbali na watani zao, Simba walionyakua mara 18.

No comments