Rooney amekuwa Manchester United tangu 2004
Meneja wa Manchester United Jose Mourinho amesema bado inawezekana Wayne Rooney aihame klabu hiyo mwezi huu.
Mshambuliaji huyo wa England mwenye umri wa miaka 31 alifunga bao lake
la 250 United mwezi uliopita na kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi
katika historia ya klabu hiyo.
Hata hivyo, kumekuwa na uvumi kwamba huenda akahamia China.
Soko la kuhama kwa wachezaji Ligi Kuu ya China litafungwa wiki ijayo.
Mourinho aliulizwa iwapo nahodha huyo wa United atakuwa Old Trafford kufikia wakati huo.
"Itabidi mumwulize mwenyewe," Mourinho alisema.
"Bila shaka siwezi kuwahakikishia (kwamba atakuwa hapa). Siwezi
kuwahakikishia kwamba nitakuwa hapa wiki ijayo, nitawezaje
kuwahakikishia kwamba mchezaji atakuwa hapa msimu ujao?"
Mkataba wa Rooney United ni wa hadi 2019 na majuzi alikuwa amedokeza
kwamba kuna uwezekano huenda asimalize muda wote huo United.
Amekuwa hapewi nafasi ya kuwa katika kikosi cha kuanza mechi msimu huu na amefunga mabao matano pekee.
Hata hivyo, Mourinho alisema Oktoba kwamba Rooney hakuwa anenda "popote"
na alisisitiza Jumanne kwamba hataki mchezaji huyo aihame Manchester
United.
"Siwezi kumsukuma - au kujaribu kumsukuma - nyota wa klabu hii ahame," aliongeza Mourinho.
"Hivyo, itabidi mumwulize iwapo anaona kama atakuwa katika klabu hii
kipindi kilichosalia cha uchezaji wake au iwapo anadhani atahama.
No comments