Header Ads

RATIBA YA VPL YAATHIRI MICHEZO YA ASFC

Dar es Salaam. Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), limesema kilichosababisha kuwapo kwa mabadiliko ya ratiba ya michezo ya raundi ya 16 ya Kombe la Shirikisho (ASFC) ni ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Alfred Lucas amesema sanjari na mchezo baina ya Simba na African Lyon, ipo michezo mingine.

Hata hivyo, TFF imetangaza mabadiliko ya mchezo kati ya Simba na African Lyon huku ratiba ya michezo mingine ikibaki kama ilivyokuwa.

Michezo mingine ya raundi ya 16 bora itakuwa ni Azam dhidi ya Mtibwa, Yanga na Kiluvya United, Kagera Sugar itapambana na Stand United huku Mighty Elephant ya Songea ikitarajiwa kucheza na Ndanda FC.

Mingine itazikutanisha Madini FC na JKT Ruvuma, Mbao FC dhidi ya Toto Africans wakati Mbeya City itakwaruzana na wapinzani wao Tanzania Prisons.

“Tuliziandikia timu zote na zimetujibu kuwa zitacheza Alhamisi, tunachosema, kubadilika kwa ratiba kunatokana na sababu mbalimbali lakini tumeangalia tarehe hizo kutakuwa na michezo ya ligi,” amesema Lucas.

Makamu Mwenyekiti wa Simba, Geofrey Nyange ‘Kaburu’ amesema klabu yake imepokea barua ya kurudishwa nyuma kwa mchezo huo.

“TFF wametutaarifu kuhusu hilo na kwa kukubaliana na wenzetu (African Lyon), tumeridhia na mchezo huo utachezwa Alhamisi,” amesema Kaburu.

No comments