Mahambuliaji Mtanzania Mbwana Samatta, jana aliiongoza timu yake ya KRC Genk kupata ushindi wa mabao 2-1 katika mbio za kuelekea kuwania kufuzu kwenye michuano ya Europa League msimu ujao.
Samatta ambaye alikuwa hajafunga katika mechi kadhaa zilizopita, alikuwa mmoja wa wafungaji kwa kutupia wavuni bao la pili wakati timu yake ilipoichakaza Eupen katika mechi ya Ligi Kuu Ubelgiji.
Nahodha huyo wa Taifa Stars alifunga bao hilo katika dakika ya 28 baada ya kupokea pasi ya Thomas Buffel, akawatoka walinzi kwa kasi kabla ya kuukwamisha mpira wavuni.
Kabla ya hapo, Genk ilikuwa ya kwanza kupata bao kupitia Jere Uronen katika dakika ya 18 akiunganisha basi nzuri ya Samatta.
Bao la Eupen liliweka wavuni na Henry Chukwuemeka Onyekuru dakika ya 76 lakini dakika ya 78 mchezaji Jere Uronen wa Gnek alilambwa kadi ya njano ya pili na kutoka nje.
Kwa ushindi huo, Genk inaendelea kuongoza Kundi B hatua ya play-off ikiwa na pointi 19 na kufuatiwa na Lokeren yenye ponti 10.

No comments